Sunday, November 29, 2015

PENZI BAHARI YA TOPE.
1.Penzi huvunja sharia, kwa mambo yalo magumu,
Zee la kuamkia, akupe umaamumu,
Tiba akikupatia, wapo wato kulaumu,...
Penzi bahari ya tope, haina mpiga mbizi.

2.Penzi huvunja sharia, zile za kimaumbile,
Kijura ukiyangia, tashika nyuma na mbele,
Zito takuinamia, hata upige kelele,
Maji yapande mlima, kwa mapenzi si neno.
3.Penzi hujenga ghorofa, pasina nguzo angani,
Mkwasi apose lofa, simba apende majani,
Maliki afe kifafa, kwa penzi la utumwani,
Nasema humpendaye, huhitaji kumsikia.
4.Penzi hupika chakula, bila moto tambueni,
Nahau Lila na Fila, ati havitengamani,
Fila kamuoa Lila, penzi lashindwa na nini?
Mja siseme hayawi, kwa penzi laweza kuwa.
5.Penzi huwa muujiza, bubu apate ongea,
Tena pia hushangaza, kiwete anatembea,
Kipofu anatangaza, mwezi amejionea,
Sishangae ndo mapenzi, bubu kuoa kipofu.
6.Penzi hutoka moyoni, si lile pande la nyama,
Penzi hisi za rohoni, ndo pumzi za mtima,
Penzi sione machoni, utakuja shika tama,
Nasema humpendaye, huhitaji kumuona.
7.Penzi si sauti nzuri, ya mahaba sikioni,
Moyo haufi kwa ghuri, zinazo kita ngomani,
Moyo ukiwa tayari, kiziwi atabaini,
Hata uwe na uziwi, sauti yake tasikia.
Dotto Chamchua Rangimoto.
Njano5.
255762845394whatpp
255784845394
 

No comments:

Post a Comment