MOYONI USHANIJAA
Penzi langu mahabuba,moyoni nimeliweka,
Penzi lililo na huba,ambalo limeniteka,
Sitalitoa nasaba,penzi langu na hakika,
Moyoni ushanijaa,moyoni ushaingia,
Maneno ya majirani,hayatonibadilisha,
Nimekupenda mwandani,sitoweza kukanusha,
Nimekuweka moyoni,hakuna anaye bisha,
Moyoni umenikaa,moyoni ushaingia,
Wewe ni tulizo langu,hakuna zaidi yako,
Umeteka moyo wangu,ninakupenda mwenzako,
Nakupa upendo wangu,sitojuta juu yako,
Moyoni umenikaa,moyoni ushaingia,
Watu washasema mengi,yanayo tuhusu sisi,
Na wala hatujitengi,wakaja tuona nuksi,
Pembeni hatusimangi,twachukulia wepesi,
Moyoni ushanijaa,moyoni ushaingia.
Sisikilize vishawishi,vya watu wa mitaani,
Kwani mi siwezi ishi bila wewe maishani,
Milele uwe mbishi nilinde wako mwandani,
Moyoni ushanikaa moyoni ushaingia.
Kamwe usinisaliti nitakuja kuumia,
Epuka hao vibinti,wasije kukuvamia,
Na hao pia madenti wazo za kwao nia,
Moyoni ushanikaa,moyoni ushaingia.
Nimekupenda kwa dhati uongo sitaongea,
Tukajaza pia cheti na ndugu kushangilia,
Tusiingize boliti tukaja tukaumia,
Moyoni ushanijaa,moyoni ushaingia.
Walitaka tutengane,ili waje shangilie,
Karibu tusionane,uongo watutungie,
Nibaki kuwa mjane,na kasha wanizomee,
Moyoni ushanijaa,moyoni ushaingia.
Wewe ni tabibu wangu,mwengine siwezi pata,
Unaponya gonjwa langu,naafuu ya kukupata,
Ukiwa karibu yangu,moyo wangu utakata,
Moyoni ushanijaa,moyoni ushaingia.
Tamati nimefikia,mpenzi ubaki name,
Wambea kuwaumbua,uishi pamoja nami,
Ili upate tambua,unipende mara kumi,
Moyoni ushanijaa,moyoni ushaingia.
No comments:
Post a Comment