Nivumilie mpenzi,katika shida na raha,
Mapenzi tuyape pumzi,yapumue kwa furaha,
Lidumu la kwetu penzi,liwe lenye nyingi siha
Nivumilie mpenzi,kwenye raha na karaha.
Penzi halina athari,subira likivutiwa,
Litakuwa machachari,mkazo likitiliwa,
Na mahaba ushamiri,bila ya kutarajiwa,
Nivumilie mpenzi,kwenye raha na karaha.
Penzi tuvumiliane,mahaba kuyafufua,
Suluhu ipatikane,kwa yanayo tusumbua,
Mengi tushirikiane,matatizo kutatua,
Nivumilie mpenzi,kwenye raha na karaha.
Nivumilie laazizi,mapenzi miangaiko,
Unipatie ujuzi,sielewi niendako,
Nina lingi jinamizi,jibu ushauri wako,
Nivumilie mpenzi,kwenye raha na karaha.
Penzi sio malumbano,penzi ni uvumilivu,
Wala sio mapigano,bali mwingi utulivu,
Penzi ni maridhiano,yenye kulitia nguvu,
Nivumilie mpenzi,kwenye shida na karaha.
Penzi si kwa masikini,wala halina chaguo,
haliitaji yakini,moyo ndio ufunguo,
likiingia moyoni,laweza kuvua nguo,
nivumilie mpenzi,kwenye raha na karaha.
Mapenzi uvumilivu,dawa ni uaminifu,
Dunia hii tulivu,kuna mengi mapungufu,
Penzi likikosa nguvu,hakuna uaminifu
Nivumilie mpenzi kwenye raha na karaha.
No comments:
Post a Comment