Sitaki umbea wala kuumbua watu. Miaka yote zikifanyika sherehe za Uhuru na nyinginezo, wasomi, wanasiasa na wananchi wa kawaida wamekuwa wakisifu maandalizi yake na kwamba zimefana. Hawakosoi.
Leo watu haohao wanamsifu Rais John Magufuli kwa kufuta baadhi ya sherehe hizo. Magazeti yanasifia tu. Fungua gazeti lolote huwezi kukosa vichwa: “Kasi ya Magufuli yatanda kila kona;” “Magufuli usipime;” “Magufuli atisha;” “Magufuli…” Hivi amefanya nini kipya, kufuta safari za nje? Je, amefuta safari au hali ya fedha inamlazimisha aangalie maeneo fulani ya kipaumbele?
Mtangulizi wake, Jakaya Kikwete alikuwa anajisifu, Magufuli anatenda ili wengine wamsifu. Ndiyo maana mara anatangaza kufuta ziara na sherehe, mara kavamia Hazina, Muhimbili, mara mikutano serikalini kufanyika kwa video, mara hakuna kuchapisha kadi kwa fedha za Serikali, mara amewamwaga vigogo TRA. Kesho yake magazeti yanampamba na kumjenga.
Ole wao watangulizi wake wadai kwamba anawaumbua! Ole wao CCM walalamikie kasi yake! Magufuli anajua watakaomnyoshea kidole watakumbana na nguvu ya umma.
Magufuli anajua alipata upinzani mkali wakati wa kampeni kwa sababu wapinzani kwa muda mrefu walijijenga kwa wananchi kwa kaulimbiu ya nguvu ya umma.
Katikati ya kampeni aliiga mbinu za wapinzani na hata kukarabati sera za CCM kuvunja zilizokuwa zinanadiwa na wapinzani. Sasa anatekeleza.
Hebu tazama suala la sherehe. Wapinzani walipojinadi mwaka 2010 na mwaka huu wakiingia madarakani watafuta baadhi ya safari za nje na sherehe halafu watauweka Mwenge wa Uhuru katika makumbusho ya Taifa, Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwashambulia kwa maneno makali. Hata wasomi wenye mrengo wa CCM waliwaona wapinzani watu wa ajabu sana.
Leo wasomi walewale waliokosoa mkakati wa wapinzani (CUF, Chadema, NCCR - Mageuzi) wa kufuta sherehe za kitaifa, ndiyo wanaompongeza Magufuli kwa anachokifanya. Sipati picha Mkapa anajisikiaje anapoona “mtoto wao mpendwa” anatekeleza sera aliyoilaani.
Kasi ya Magufuli imesababisha wasaidizi wa wilayani wanaumiza watu. Novemba mwaka jana akiwa Kamanda wa Uhamasishaji wa UVCCM, Paul Makonda anadaiwa ‘kumlamba za uso’ aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu, Joseph Warioba. Waliolaani utovu ule wa nidhamu ni wapinzani na wanaharakati tu.Mapema mwaka huu akateuliwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Wiki hii akatangaza kuwasweka mahabusu kwa saa sita maofisa ardhi 20 wa manispaa hiyo kwa kuchelewa kuwasili katika ziara ya kutatua migogoro ya ardhi katika manispaa hiyo.
“Hii haikubaliki hata kidogo. Mimi niliwasili kwa wakati, Ofisa Tawala wa Wilaya (Das) aliwasili kwa wakati na hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni aliwasili kwa wakati. “Tulilazimika kuwasubiri (maofisa ardhi) kwa saa tatu nzima hadi saa tano asubuhi kwa sababu bila wao hakuna kitu ambacho kingefanyika,” alisema.
Makonda alidai baada ya kubaini muda uliosalia usingetosha kufanya ziara hiyo, alilazimika kuiahirisha na kuamuru kukamatwa maofisa hao kwa kile alichodai kosa la dharau na kukosa heshima kwake akiwa kiongozi. Alisema uamuzi huo aliufanya ndani ya sheria kama Mwenyekiti wa baraza la ulinzi na usalama la wilaya hiyo.
Hivi kitendo cha Makonda kutangaza ‘kulostisha’ maofisa ardhi kwa saa sita mahabusu kwa kuchelewa ndiyo njia ya kuchochea kasi ya uimarishaji utumishi wa umma au ndiyo utekelezaji wa kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu ya Magufuli?” Je, Makonda ni mamlaka ya nidhamu?
Baadhi wamefurahia hatua hiyo, lakini nadhani Magufuli hatafurahi kiongozi kutumia vibaya madaraka. Kama ni mchapakazi kwa nini hali imefikia hapo? Si anastahili kuadhibiwa kama Kikwete alivyofanya.
Februari 2009, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Bukoba, Albert Mnali aliamuru walimu 32 wachapwe viboko kwa madai walisababisha wanafunzi kufeli katika shule za msingi zilizoko Bukoba Vijijini. Alifukuzwa kazi; siku hizi ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nachingwea. Aprili 2010, Sungusungu wa Shinyanga wakaamua kuwacharaza bakora walimu wanne akiwamo mwalimu mmoja mwanamke ambaye alikuwa ni mjamzito kwa kosa la kuchelewa kwenye kikao cha walimu na wazazi. Sungusungu hao nao walishughulikiwa. Vipi Makonda?
Haya Polisi wa Mwanza, wanahangaika kuzuia kuagwa maiti. Wameacha kazi ya kulinda amani na usalama wanazuia watu wasikusanyike kuaga maiti ya mpendwa wao aliyeuawa kwa kuchinjwa na watu wanaodaiwa kuwa makada wa CCM. Mwanasheria wa Serikali anajitokeza kudai eti marehemu Alphonce Mawazo asiagwe Mwanza kwa vile si kwao. Kweli Serikali inathubutu kutoa madai ya kibaguzi kama haya? Wanaodhani wanamridhisha Magufuli wataumbuka. Tusubiri.
No comments:
Post a Comment